Thursday, September 02, 2010

LAU LIMEMGEUKIA



JITIHADA za Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi na mbunge anayemaliza muda wake katika Jimbo la Nyamagana, Lawrence Masha, za kupita bila kupingwa katika kinyang’anyiro cha ubunge katika jimbo hilo zimegonga mwamba baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutengua uamuzi wa awali wa msimamizi wa uchaguzi kumzuia mgombea wa CHADEMA.

Taarifa zinadai kuwa NEC imeamua kumrejesha mgombea wa CHADEMA, Ezekiah Wenje ambaye alikuwa wakifanya kazi NMG hapa Harbour View jijini Dar es Salaam, baada ya kuridhishwa na vielelezo vya uraia wake.

Kurejeshwa kwa Wenje katika kinyang’anyiro hicho kitazidisha chachu ya uchaguzi wa ubunge, ambayo tayari ilionekana kutokuwa na msisimko baada ya Masha kuwa mgombea pekee.

NEC leo itatangaza uamuzi huo ambao umepokewa kwa hisia mbalimbali na baadhi ya wakazi wa Jimbo la Nyamagana na wafuatiliaji wa masuala ya siasa.

Waziri Masha aliwasilisha pingamizi dhidi ya Wenje kwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Wilson Kabwe, ambaye aliridhika na nyaraka zilizowasilishwa na waziri huyo, hivyo kuamua kumuengua mgombea huyo.

Baada ya uamuzi huo, Wenje aliamua kukata rufaa NEC kwa kuambatanisha vielelezo vyake kuthibitisha kuwa ni raia wa Tanzania na si raia wa Kenya kama Waziri Masha alivyodai.

Mmoja wa viongozi wa juu wa CHADEMA alithibitisha kuona barua ya NEC, ikiwaarifu kulitupa pingamizi lililowekwa na Waziri Masha, hivyo kumruhusu Wenje kuanza pilikapilika za kampeni.

kiongozi huyo ambaye hakupenda jina lake litajwe kwa misingi kuwa si msemaji wa chama hicho, alisema tayari wameshaanza maandalizi ya kampeni na wana uhakika wa kumbwaga tena Waziri Masha katika kinyang’anyiro hicho.

“Ni kweli NEC imemrejesha mgombea wetu baada ya kuona vielelezo vilivyotolewa na mgombea wa CCM vina upungufu na vya mgombea wetu kuwa ni sahihi… tunaamini kwamba haki imetendeka na kinachofuata ni mapambano sasa,” alisema kiongozi huyo

No comments: