Friday, September 17, 2010

TAA ZA SOLAR KWA MAISHA BORA

Balozi wa ' Haki ya Mwanga Salama' Msanii Mrisho Mpoto akielezea juu ya wimbo wake wa mama Siwema kinachohamasisha matumizui ya taa za umeme wa jua.
Mrisho na wasanii wenzake wakuburudisha waalikwa wakati wa uzinduzi wa wimbo huo, Mamam Siwema.

Mpoto akionyesha taa ya umeme jua (Solar) ambayo ilizinduliwa kwa ajili ya wanafunzi wa shule mbalimbali kwa ajili ya kujisomea ambapo watapata kwa ofa ya Sh 10,000 tu. kulia ni mgeni rasmi, Katibu Mkuu wa Basata ambaye ni katibu


Femina HIP kwa kushirikiana na D.light, kampuni inayotengeneza na kusambaza taa zinazotumia nishati ya jua, wanahamasisha jamii kuhusu matumizi ya taa hizo na kuhakikisha upatikanaji wake. Kwa kutambua umuhimu huo Femina Hip imezindua kibao maarufu cha msanii wa mashairi, Mrisho Mpoto, kinachokwenda kwa jina ‘Mama Siwema’.

Kibao hiki kinahamasisha matumizi ya taa za sola ambazo ni salama kwa mtumiaji na rafiki kwa mazingira. Tuna furaha kuwaalika wanahabari na wadau muhimu katika hafla hii. Karibu tuburudike kwa muziki, tupate picha ya video kwa pamoja na kisha tujadiliane kuhusu taa za sola.

Mwezi Januari 2010, Femina HIP na D.light kwa pamoja tulizindua kampeni ya kitaifa ya ‘Haki ya Mwanga Salama’. Lengo la kampeni ni kuchochea mabadiliko ili hatimaye shule zote, wanafunzi, wazazi na serikali watafakari na kuunga mkono matumizi ya taa za sola. Mkurugenzi Mtendaji wa Femina HIP, Dk Minou Fuglesang, anasema: “Tungependa kuona wanafunzi wote wanapewa vitabu, kalamu, sare za shule lakini pia wanapatiwa taa salama ili waweze kujisomea na waboreshe maisha yao”.

Shughuli mbalimbali za uelimishaji zimefanyika ikiwa ni sehemu ya kampeni hii. Mrisho Mpoto, msanii maarufu wa mashairi, ni balozi wa kampeni ya “Haki ya Mwanga Salama”. Amekuwa akitoa burudani kwa jamii nchini kote, huku akizungumzia faida za taa za sola. Hivi sasa ametunga wimbo “Mama Siwema” ambao unaelezea hadithi ya Siwema, mwanafunzi wa sekondari aliyekuwa na bidii ya hali ya juu masomoni, ambaye alipoteza maisha yake katika ajali ya moto wakati akijisomea kwa kutumia taa ya mafuta (chemli).

Mrisho aliguswa sana na janga la moto lililotokea katika shule ya bweni ya Idodi mwaka jana, ambapo wanafunzi wa kike 12 walipoteza maisha. Moto huo ulisababishwa na mojawapo ya mishumaa ambayo wanafunzi walikuwa wakiitumia kwa kujisomea, huku wakiwa wamekaa katika vitanda vyao.

Tukio hilo lilimpa hamasa ya kutunga wimbo huu ili kuuamsha umma kutambua kwamba tunaweza kuepuka majanga ya namna hiyo. Ajali kama hizo zinaweza kuepukwa ikiwa wanafunzi watapata mwanga salama wa taa za sola.

Anatumaini kwamba wimbo wake utaelimisha jamii kuhusu taa za sola na hatari za taa zinazotumia mafuta ya taa, na kwamba walimu, wazazi na wanafunzi wenyewe wataelewa hatari ya matumizi ya mafuta ya taa. Zaidi ya hayo, Mrisho anaamini kwamba kibao chake hicho kitachochea jamii kutafuta na kutumia nishati mbadala ambazo hivi sasa zinapatikana nchini Tanzania.

Anaeleza: “Kila mwanafunzi nchini Tanzania ana haki ya kujisomea kwa kutumia mwanga salama wa taa za sola. Shuleni panapaswa kuwa ni mazingira salama kwa vijana wa nchi hii. Kwa kampeni ya “Haki ya Mwanga Salama” tunajitahidi kuhakikisha jamii inaifanyia kazi changamoto hiyo”.

Ukosefu wa vyanzo salama vya nishati ni changamoto kubwa inayoikabili Tanzania, kwani 10% tu ya wananchi ndio wenaofikiwa na huduma ya umeme. Maeneo ya vijijini, ni 2% tu. Lakini leo hii kumekuwa na ongezeko la upatikanaji wa vifaa vinavyotumia nishati ya jua na taa zinazotumia nishati hiyo, ambazo hata wananchi wa vijijini wanamudu gharama yake.

Teknolojia hiyo hivi sasa ipo na kuna haja ya kuhamasisha matumizi yake katika jamii. Femina HIP na D.light kwa pamoja tunatoa mchango wetu muhimu katika kuhakikisha kwamba jamii ya Tanzania inaelimika na kutumia taa za sola ili kuboresha kiwango cha elimu kwa kuwawezesha wanafunzi kujisomea katika mazingira salama, kuishi mtindo bora wa maisha na kuboresha maisha ya jamii nzima.

Katika hafla hii, D.light imezindua ofa maalumu ya taa ya kusomea ‘Solata’ kwa shule za sekondari nchini Tanzania. Wanafunzi 50 kwa kila shule ya sekondari wataweza kupata taa ya sola ya kusomea, yenye thamani ya Tsh 22,500 kwa bei pungufu ya Tsh 10,000 TU! Vocha maalumu zitasambazwa sambamba na toleo lijalo la Jarida la Fema ambalo litasambazwa mwezi Oktoba.

Kwa habari zaidi wasiliana na frederick@feminahip.or.tz ama laura.smeets@dlightdesign.com

No comments: