Thursday, September 23, 2010

TENDWA LIMEMFIKA

HATIMAYE Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, amenyoosha mikono na kusalimu amri huku akikiri kuingilia mamlaka ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kudai kamwe hatajiuzulu kwa kelele za wanasiasa.

Tendwa alieleza kuhusu mkanganyiko ulioibuka kutokana na tamko lake kwamba muda wa kumaliza kampeni ulikuwa umesogezwa kutoka saa 12:00 za awali hadi kufikia saa 1:00 jioni.

Akifafanua Tendwa alisema kisheria tume ndiyo ilistahili kutoa taarifa ya mabadiliko ya muda wa kumaliza kampeni, ingawa hawakufanya hivyo.Awali ilidaiwa kuwa Mgombea wa CCM Jakaya Kikwete amekuwa akiendesha mikutano ya kampeni hadi saa moja usiku kinyume na utaratibu wa Tume ya Uchaguzi ambapomikutano huwa mwisho sa 12 jioni.

“Ni kweli ninakiri niliteleza katika tamko langu… mimi sina ugomvi na wenzangu wa NEC, hili linaweza kumtokea binadamu yeyote pamoja na mkanganyiko huu… wadau wa uchaguzi huu wanaelewa tulivyokubaliana kuhusu suala la muda,” alisema Tendwa.Hata hivyo alipotakiwa kueleza lini na vyama gani alikutana navyo kujadili kuhusu kuongeza muda, Tendwa alishindwa kufanya hivyo na kuhitimisha maelezo yake kwa kusema alikuwa hakumbuki siku.

Aidha, msajili huyo ambaye tamko lake la awali lilisababisha mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, amtake ajiuzulu, hakuwa tayari pia kuvitaja kwa majina vyama alivyokutana navyo kujadili suala hilo.

“Sikumbuki ni lini nilikutana nao, ila nakumbuka tulikutana na wadau wote. Bado nasisitiza na kukwambia mimi sina ugomvi na NEC, ni kweli wao ndio wenye mamlaka hayo,” alisisitiza Tendwa.

No comments: