Monday, November 29, 2010

GURUMO TAABANI

HALI ya mwanamuziki nguri na kiongozi wa bendi ya Msondo ngoma, Muhidin Maalim Gurumo anayesumbuliwa na tatizo la maji kujaa katika mapafu, hali inazidi kuwa mbaya na sasa amehamishiwa wodi namba moja na kuwekwa chini ya uangalizi wa karibu wa daktari.

Mwanamuziki huyo awali alilazwa katika wodi namba tano katika hospitali Muhimbili tangu alipofikishwa hapo wiki iliyopita, lakini kutokana na hali yake kuzidi kubadilika sasa amehamishia ICU na kuwekwa chini ya uangalizi wa karibu wa daktari na wauguzi.

Muuguzi wa zamu katika hospitali hiyo ambaye hakupenda jina lake kuchapwa gazetini kwa kuwa si msemaji alibainisha kuwa hali ya mzee Ngurumo si nzuri na kinachofanyika hivi sasa ni kujaribu kuyaondoa maji ambayo yamejaa katika mapafu yake kwa kutumia mashine maalum.

Mwananchi lilifika wodini hao wakati wa kuona wagonjwa jana lakini wakati wote alikuwa amelala na mara moja moja alipepesa macho na kurudi tena usingizini na wauguzi waliokuwa zamu walieleza kuwa kuna mtoto na mke wake ambao wanapeana zamu za kumhudumia hospitalini hapo.

"Tuombe Mungu kwani huu ni ugonjwa wa kawaida na wengi huwa wanapona kikubwa hapa ni kumhakikishia kuwa anapata huduma za uhakika na zinazofaa" alisema muuguzi huyo na kuongeza kuwa kinachoonekana ni kuwa msaada zaidi unahitajika.


No comments: