Friday, January 07, 2011

PEOPLES POWER!!!




UMATI wa wakazi wa mkoa wa Arusha na maeneo ya jirani, jana ulifurika katika Viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya rusha, kusikiliza kesi iliyokuwa inawakabili viongozi wa Chadema, akiwamo Mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa.

Vingozi hao pia walifikishwa mahakamani hapo sambamba na wabunge watatu wa chama hicho; Philemon Ndesamburo wa Moshi Mjini, Joseph Selasini wa Rombo, Godbles Lema wa Arusha na watu wengine 21.

Kwa pamoja walifikishwa katika viwanja vya Mahakama Kuu majira ya 8:40 mchana wakiwa chini ya ulinzi mkali, huku Dk Slaa, Mbowe na Mbunge wa jimbo ya jimbo la Moshi mjini, Filemon Ndesamburo wakiwa kwenye gari dogo aina ya Landrover.

Watuhumiwa wengine walifikishwa mahakamani hapo kwa karandinga.
Waliokuwa kwenye Karandinga hilo ni Selasini, Lema na washitakiwa wengine wote waliobaki.

Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Zakaria Elisante alimweleza Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha Charles Magesa, kuwa watuhumiwa hao, wametenda kosa moja la kufanya mkusanyiko kinyume cha sheria.

Elisante alisema kwa kufanya kosa hilo, watuhumiwa hao, wamevunja sheria namba 74 na 75 kifungu cha 16 kama ilivyofanyiwa marekebishoa mwaka 2002 na pia sheria ya polisi sura 45 kifungu cha 322 ambayo pia ilifanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Hata hivyo, watuhumiwa wote walikana makosa hayo na mawakili wa serikali alisema hana pingamizi na dhamana yao.

Mawakili wa utetezi, Method Kimomogoro na Arbert Msando, walieleza mahakama kuwa watuhumiwa wote wana wadhamini ambao baadaye walidhaminiwa kwa thamani ya Sh 2 milioni kila mmoja.

Hata hivyo, waliosomewa mashitaka jana walikuwa ni watuhumiwa 29 pekee baada ya watuhumiwa wawili kukosekana hospitali ya mkoa ya Mount Meru walipokuwa wamelazwa.Watuhumiwa hao ni Frank Rogati na Swalehe Salum.

Mchumba wa Slaa
Mchumba wa Dk Slaa, Josephine Mushumbuzi na watuhumiwa wengine watatu jana walisomewa mashitaka wakiwa katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru wanakoendelea na matibabu yao.

Josephine tayari alikuwa ameshonwa nyuzi saba kichwani na huku watuhumiwa wengine Kenedy Bundara, Juma Wambura na Richard Mtui ambao wote walikuwa na majeraha ya risasi.

Lakini wote walipewa dhamana kama wenzao waliofikishwa mahakamani na kesi hiyo imepangwa kutajwa tena Januari 21 mwaka huu.

Nahodha:

Katika hatua nyingine Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha amesema vurugu zilizotokea Arusha juzi ni tatizo la kisiasa ambalo pia litapaswa kushughulikiwa kisiasa.

“Wote tunapaswa kulinda amani yetu. Tunapaswa kutuliza hali ya Arusha. Kilichotokea Arusha ni mgogoro wa kisiasa tutautatua pia kisiasa,” alisema Nahodha alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, jana, jijini Dar es Salaam.

“Biblia inasema ‘ni heri wapatanishi kwani wao watarithi nchi,’… sisi (serikali) tutawakutanisha pande zote ili tufikie muafaka na kutuliza hali ya Arusha,” alisema Nahodha.

Alisema hatua hiyo ya maridhiano kwa sasa ni muhimu kwani, baada ya msuguano wa takribani wiki, pande mbili zinazosuguana mkoani humo, sasa zimeridhika kuwa kuna tatizo la msingi ambalo linapaswa litatuliwe.
“Kunawakati wa kuchukia na wakati wa kufurahi, wakati wa kupenda na wakati wa kuridhiana, sasa wakati wa maridhiano umewadia,” alisema Nahodha ambaye pia anataaluma ya Udpolomasia.


Aliendelea kufafanua kuwa, kulingana na taaluma ya migogoro, usuluhishi hufanikiwa pale tu ambapo wahusika wa pande zinazosuguana kuona na kuamini kwamba kuna tatizo.

Alisema kuwa, kwa muda sasa zilikuwepo juhudi za kusuluhisha mgogoro wa Arusha, ambazo zilikuwa zikifanyika chini chini, lakini kutokana na hali ilivyo sasa, itabidi usuluhishi huo kufanyika kwa uwazi.

Kuhusu muda utakaotumika kufanya usuluhishi huo kisiasa, Nahodha alisema “Nadharia ya usuluhishi wa migogoro kwanza kabisa ni kutokuwa na haraka, suala la muda utakao tumika, utategemeana na msuluhishi pamoja na wasuluhishwaji. Unaweza kutumika hata second (sekunde) moja.”

Akijibu swali kama serikali itakuwa tayari kufuta kesi mbalimbali zinazowakabili viongozi na wananchi waliokamatwa kutokana na tukio hilo, Naodha alisema hakuna na jibu la moja kwa moja ingawa swali hilo litachukuliwa kama ushauri.

Kuhusu uwezekano wa kutengua matokeo ya umeya Arusha, suala ambalo pia Chadema wanalilalamikia, Naodha alisema “Sina uhakika kama tatizo la msingi lililopo Arusha linatokana na Umeya. Lakini katika mazungumzo tukibaini kuwa hilo ndiyo tatizo basi tutalifanyia kazi.”

IGP Mwema Kigugumizi
Naye IGP Said Mwema ambaye pia alikuwepo katika mkutano huo, alionekana kupata shida ya kujibu maswali mengi yaliyoulizwa na waandishi juu ya polisi kutumia nguvu nyingi.

Alikwepa kujibu pia swali la waandishi wa habari iwapo kuna polisi anayeshikiliawa kutokana na kusababisha vifo vya raia wawili.

Waandishi waliuliza maswali baada ya Waziri Naodha kumaliza kuzungumza, ambapo baada ya kuyaandika maswali ya waandishi alimtaka IGP kuanza kutoa majibu kwa yale maswali yanahusu moja kwa moja polisi.

Katika awamu ya kwanza ya kujibu maswali hayo, IGP hakujibu swali lililomtaka kueleza endapo madhara yaliyotakana na fujo hizo, ni madogo, makubwa au yanalingana na yale ya taarifa alizodai kuwa ni za kiintelijensia, ambazo walizitumia kutoa tamko la kisitisha maandamano.

Kuhusu madai kwamba kuna kikosi cha polisi kutoka Ukonga jijini Dar es Salaam, Chuo cha Polisi Moshi (CCP) na Manyara vilivyopelekwa Arusha kudhibiti vurugu, alisema:

“Hakuna askari tuliowachukua sisi kutoka Ukonga, suala la polisi kutumia askari wangapi na kutoka wapi, hilo ni suala la taaluma ya polisi na hatuwezi kutangaza kwa kuwa hayo ni mambo ya security (kiusalama)."

Hata hivyo alisema kuna wana askari wa ziada na akakiri kuwai kuna vikosi vingine vilipelekwa Arusha juzi ili kuongeza nguvu ya kulinda usalama wa raia kuanzia jana.

“Sisi kuweka mpaka askari wa reserve (waakiba) mngetupongeza, kuongeza askari sisi hiyo ni issue ya kiusalama, kuna mpaka askari waliondoka jana (juzi) kwa sababu ya ku-project hali leo (jana).

Alisema kutokana na hali ilivyo katika mkoa huo, maafisa mbalimbali wa polisi walitumwa kwenda Arusha ili kuchunguza hali ilivyo.

Juu ya kuwepo kwa mkanganyiko wa amri ya kamanda wa polisi mkoa wa Arusha ya kuruhusu maandamano pamoja na aliyoitoa ya kusitisha amaandamano, IGP.

“Kwa taarifa yenu kuna barua ya ruhusa na katazo la maandamano hayo kutoka kwa RPC wa Arusha, nilichokifanya mimi ni kutoa msisitizo tu,” alisema IGP Mwema.

No comments: