Friday, January 25, 2008

GARI LA WAZIRI WA USALAMA WA RAIA



GARI la Naibu Waziri wa Usalama wa Raia, ambalo liliporwa Jumamosi wiki iliyopita limepatikana likiwa limetelekezwa katika Ofisi za Chama Cha Mapinduzi Tawi la Kimanga, Tabata Dar es Salaam.
Gari hilo lilikutwa jana jioni na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) tawi la Wizara ya Usalama wa Raia, Arcado Nchinga na kulitilia shaka alipokuwa akipita eneo hilo kwenda kumsabahi ndugu yake.
"Mwenyekiti wetu wa Tughe aliliona gari likiwa limeegeshwa hapo na kwa kuwa alikuwa analifahamu, alitufahamisha ofisini na kuulizia namba zake na tulipomtajia aligundua kuwa ndilo," alieleza afisa mmoja wa wizara hiyo.
Alisema baada ya kujiridhisha aliamua kutoa taarifa polisi na baadaye polisi walilivamia eneo hilo na kukuta gari likiwa limeegeshwa huku likiwa limefungwa milango, na mlingoti wa bendera kung’olewa.
Taarifa zilizopatikana katika ofisi za CCM lilipokutwa gari hilo zilieleza kuwa, liliegeshwa na watu wasiojulikana Jumapili saa nne usiku na hawakurudi tena kulichukua hadi lilipokutwa leo.
Katika eneo la tukio, wataalamu wa alama za vidole kutoka Jeshi la Polisi walikuwa wakifanya kazi ya kutambua alama katika gari hilo na tukio hilo lilivuta umati wa watu wa maeneo ya jirani, na Kamati ya Siasa ya Tawi hilo ililazimika kukutana ghafla.

No comments: