Shahidi wa sita katika ya kina Zombe, Mjatta Kayamba mkazi wa Sinza C, Palestina ameweza kuwatambua watuhumiwa wawili katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wa madini waliouawa Januari 14, 2006 jijini Dar es Salaam wakidhaniwa kuwa ni majambazi.
Shahidi huyo alimtambua mtuhumiwa namba tatu ASP Ahmed Makele na mtuhumiwa wa tano WP.4593 Jane Andrew kwamba walihusika katika tukio hilo.
Akitoa ushahidi huo mbele ya Jaji Salum Masatti wa Mahakama Kuu ya Tanzania, anayesikiliza kesi hiyo, shahidi huyo alidai askari hao ni miongoni mwa askari watatu waliofika Sinza Palestina karibu na nyumbani kwa Mathew Ngonyani ambako wafanyabiashara hao walikuwa wamekwenda.
Kayamba alidai kuwa, siku hiyo akiwa nyumbani kwake, aliwaona wafanyabiashara hao wakielekea nyumbani kwa Ngonyani wakiwa na gari dogo na kusalimiana na mke wa Ngonyani na muda mfupi baadaye wakati wafanyabiashara hao wanataka kuondoka, ilifika gari aina ya Toyota Stout na kuzuia gari ya wafanyabiashara hao kuondoka kwenye eneo hilo.
“Mara walishuka askari kama watano hivi, huku wawili wakiwa wamevaa sare na wengine watatu wakiwa na silaha mkononi na kuwaamuru wafanyabiashara hao washuke ndani ya gari lao kwa madai kuwa ni majambazi,”alieleza Kayamba.
Alidai baada ya wafanyabiashara hao kushuka, askari hao walianza kuwapekua na kuchukua simu zao na kwenda kufungua buti la gari la watuhumiwa na kukuta ‘Briefcase’ (mkoba) ambayo ndani yake kulikuwa na mfuko wa nailoni uliokuwa na pesa.
Alidai kuwa muda mfupi baadaye ilikuja gari nyingine aina ya Toyota Corolla ikiwa na askari watatu, wawili kati yao wakiwa ni wanaume na mmoja mwanamke na kwamba walikuwa wamevalia fulana nyeusi na suruali nyeusi aina ya jeans na mwingine akiwa amevaa suruali ya bluu iliyopauka na kuungana na wale askari wa awali na kuendelea kuwapekuwa wafanyabiashara hao.
“Niliweza kuwakariri askari hao, wawili kati ya watatu waliokuja nao baadaye ni yule pale wa pili na yule wa tano,” alisema shahidi huyo huku akiwaonyesha kwa kidole watuhumiwa aliowatambua.
Kayamba alisema baada ya wafanyabiashara hao kupekuliwa walifungwa pingu na
kuingizwa katika gari la askari hao na kupelekwa kusikojulikana, kabla ya kupata
habari za kuuawa kwao.
“Niliporudi kesho yake kutoka katika shughuli zangu jirani yangu Benadetha aliniambia
kuwa wafanyabiashara wale walikuwa wameuawa na baadaye usiku niliona kwenye runinga
wakitangaza kuwa wafanyabiashara hao wameuawa,” alisema.
No comments:
Post a Comment