Deus Mallya akosa mdhamini
*Arudishwa tena rumande
DEUS Mallya (27), anayekabiliwa na kesi ya kuendesha gari kwa mwendo wa kasi na kusababisha kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, amerejeshwa tena mahabusu kutokana na kukosa mdhamini licha ya dhamana yake ya Sh 5 milioni kuwa wazi.
Mallya ambaye jana alipandishwa kizimbani kwa mara ya pili, anakabiliwa na mashtaka mawili ya makosa ya usalama barabarani namba 103 ya mwaka 2008, ambayo ni kuendesha gari kwa mwendo wa kasi na kusababisha kifo cha Wangwe; na kuendesha gari bila leseni.
Mtuhumiwa huyo anadaiwa kutenda makosa hayo Julai 28, mwaka huu saa 2:30 usiku katika eneo la Pandambili, wilayani Kongwa mkoani Dodoma.
Akisoma jalada la kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi mjini hapa jana, Mwendesha Mashtaka, Mratibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Policarp Urio, aliieleza mahakama kuwa, uchunguzi bado unaendelea.
Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mkazi Mfawidhi Moses Mzuna, alisema dhamana ya mtuhumiwa iko wazi.
Hata hivyo, licha ya mahakama kutoa fursa hiyo ya dhamana kwa mshtakiwa, hakukuwa na mtu aliyeweza kujitokeza kumdhamini. Hadi mwandishi wetu anaondoka mahakamani hapo, mtuhumiwa alikuwa amerejeshwa mahabusu katika gereza la Isanga.
Katika masharti hayo ya dhamana, Hakimu Mzuna, alifafanua kwamba, Mallya anatakiwa kudhaminiwa na mtu mmoja aliyetakiwa kusaini dhamana hiyo yenye gharama ya kiasi hicho cha fedha.
Hakimu alimtaka mshtakiwa huyo kujieleza iwapo alikuwa na mtu wa kumdhamini, na Mallya alimtaja kaka yake anayeitwa Priscus Mallya, ambaye alikuwa katika viwanja hivyo, ingawa hakuonekana ndani ya mahakama.
Awali, Mallya aliingia mahakamani akionyesha kujiamini na hata alipomsikiliza hakimu alikuwa makini.
Mallya alifikishwa mahakamani hapo saa 3:00 asubuhi na kisha dakika tano baadaye akapanda kizimbani.
Kesi hiyo ambayo uchunguzi wake haujakamilika, ilitumia muda wa takriban dakika 5 toka kutajwa hadi kuahirishwa, ikiwa ni pamoja na muda wa kumsubiri mdhamini wa Mallya.
Kesi hiyo itatajwa tena Agosti 28, mwaka huu baada ya kusomewa mashtaka yake Agosti mosi.
No comments:
Post a Comment