Thursday, September 25, 2008

ZOMBE LEO

Wakili ataka naibu waziri aitwe mahakamani

WAKILI wa upande wa utetezi, Moses Maira ametaka aliyekuwa Naibu Waziri wa Usalama wa Raia ajumuishwe katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa Mahenge na dereva teksi inayomkabili aliyekuwa mkuu wa upelelezi wa mkoa wa Dar es Salam (ACP), Abdallah Zombe na wenzake 12.

Maira alitoa kauli hiyo jana katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam wakati shahidi wa 35, ambaye ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Sigine Mkumbi alipokuwa akitoa ushahidi katika kesi hiyo.

Maira, ambaye anamtetea Zombe, alimuuliza shahidi huyo "kwanini Zombe anashitakiwa kwa kosa la kutangaza habari za mauaji" wakati aliyekuwa naibu waziri wa usalama wa raia wakati huo hakufikshwa katika mahakama hiyo kwa mauaji.

“Baada ya Zombe kutangaza kwenye vyombo vya habari kuhusu mauaji hayo, jioni ya siku hiyo hiyo, naibu waziri wa usalama wa raia naye alitangaza habari hizo hizo lakini hajaletwa mahakamani,” alidai Maira.

Shahidi huyo alijibu kuwa Zombe amefikishwa katika mahakama hiyo baada ya upelelezi kufanyika.

Maira na Wakili Jerome Msemwa, wanaotetea washtakiwa, jana walionekana kuhaha kumuokoa Zombe wakati wa kuuliza maswali na wakati wote Zombe alionekana akiandika vikaratasi na kuwapa mawakili wake au hata kuwaita na kuwanong’oneza.

Baadhi ya maswali yaliyoulizwa na mawakili hao yalizua vicheko katika mahakama hiyo na kuna wakati Jaji Kiongozi, Salum Massati aliingilia kati na kuwataka waendelee na maswali mengine.

Akiongozwa na kiongozi wa jopo la mawakili wa serikali, Mugaya Mutaki, shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa anafanya kazi makao makuu ya upelelezi polisi, kitengo kinachoshughulikia makosa dhidi ya binadamu.

Alieleza kuwa Februari 18, mwaka 2006 aliitwa na mkurugenzi wa zamani wa upelelezi wa makosa ya jinai, Adadi Rajabu na kumuagiza kuwa atasimamia upelelezi wa kesi ya mauaji ambayo polisi waliwaua majambazi.

Alidai Februari 20, mwaka 2006 waliwapeleka watuhumiwa nane mahakamani na kwamba watuhumiwa saba walikuwa bado hawajakamatwa.

Shahidi huyo alidai Machi 3 mwaka 2006, alikuwa ofisini kwake na aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ACP Alfred Tibaigana alimpigia simu na kumjulisha kuwa kuna mtuhumiwa ambaye anatafutwa na kwamba mshitakiwa huyo alitaka kujisalimisha.

“Alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Ahmed Makele ambaye alikuwa mkuu wa upelelezi wa kituo cha polisi cha Urafiki na mimi nilimjibu niko tayari kwa kazi,”alidai Mama Mkumbi.

Alidai mshitakiwa huyo alipofikishwa kwake alimuuliza kama yuko tayari kutoa maelezo yake na alimjibu kwamba yuko tayari.

“Nilimuhoji alikokuwa awali na kwanini aliamua kujisalimisha akasema alikuwa ameenda nchini Misri kikazi na aliporudi alisikia anatafutwa ndipo akaamua kujitokeza,” alidai Mama Mkumbi.

Shahidi huyo alidai Machi 6, mwaka 2006 Tibaigana alimpigia tena simu na akamwambia kuwa kuna mtuhumiwa Rashidi Lema (mshitakiwa wa 11) anataka kujisalimisha.

Alisema baada ya mshitakiwa huyo kupelekwa kwake walimuuliza alikuwa wapi muda wote na kwanini aliamua kujisalimisha.

“Tulipomuuliza alisema alikuwa mafichoni na kwamba alijisalimisha kwa sababu roho ilikuwa inamsuta na kule mafichoni alikokuwa watu walitaka kumlisha nguruwe,” alisema Mama Mkumbi.

Alidai baada ya kumaliza kufanya uchunguzi, alituma jalada kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Mei mwaka 2006 na kurejeshwa kwake na hivyo DPP kuagiza maelezo ya Zombe yaandikwe.

Alidai alipomuita Zombe kwa ajili ya kuchukua maelezo yake Zombe alikataa kuhojiwa na kuwaambia kuwa kama wanataka maelezo yake, waende wakachukue maelezo aliyoyatoa awali kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP).

“Mimi sikuridhika nilimuuliza hayo kwa IGP ni yapi akaniambia 'kwani hujui kama mimi nimewajibishwa kinidhamu',”alidai Mama Mkumbi.

Huku akiongea kwa kujiamini, shahidi huyo alidai kuwa alimwambia Zombe yeye kama RCO lazima aandike maelezo, lakini alivyoendelea kubisha hakubishana naye.

“Nilikwenda kwa DCI nikamweleza akashauri kama inawezekana nimuite Zombe ili apewe taarifa na DCI mwenyewe,” alidai Mama Mkumbi.

Alidai baada ya siku mbili kupita aliitwa ofisini kwa DCI na kwamba alimkuta Zombe ofisini huko na akaambiwa aandike maelezo yake.

Mama Mkumbi alidai alimweleza DCI kuwa kwa sababu Zombe ni afisa wa polisi mwenye cheo kikubwa, aandike maelezo yake mwenyewe na Zombe alitii na kuandika.

Alidai baada ya Zombe kuandika maelezo hayo, aliyatuma kwa DPP pamoja na yale ya mshitakiwa wa 12, Koplo Rajabu Bakari.

“Nikiwa mkoani kwa kazi maalum nilimwona Zombe kupitia kwenye vyombo vya habari anapelekwa mahakamani hapo ndio nikajua amepelekwa mahakamani,” alidai Mama Mkumbi.

Shahidi huyo alidai hadi sasa washitakiwa watatu James, Frank na Koplo Saad bado hawajui walipo na kwamba wanaendelea kutafutwa.

Alidai katika uchunguzi wao, walibaini waliouawa hawakuwa majambazi na kwamba waliuawa katika msitu wa Pande.

“Tulibaini pia marehemu walikamatwa bila kuwa na mapambano ya kurushiana risasi,”alidai Mama Mkumbi.

Shahidi huyo pia alidai kuwa ushahidi wa mshitakiwa wa 11 na 12 na maelezo mengine ya mashahidi, yalimwezesha DPP kumfikisha Zombe mahakamani.

Mahojiano baina ya Wakili wa Serikali, Mutaki na mawakili wa upande wa utetezi Maira na Msemwa yalikuwa kama ifuatavyo.

Wakili: Ni nani katika timu yenu alimuhoji Zombe?

Shahidi: Hakuna aliyemuhoji kwa sababu nilimuita akakataa akasema nikachukue maelezo aliyoyatoa kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP).

Wakili:
Una ushahidi wowote wa Zombe kukataa kuandika maelezo?

Shahidi: Hakuna.

Wakili: Unajua tume ya Jaji Kipenka ilisemaje?

Shahidi: Ilisema Zombe achukuliwe hatua za kinidhamu na askari wengine 15 washitakiwe.

Wakili: Inawezekana vipi Zombe atangaze walikamata Sh 5 milioni katika tukio la uporaji fedha za Kampuni ya Bidco halafu wewe unasema kuna watu walipora fedha hizo na kugawana?

Shahidi: Sijui hilo, Zombe anaweza kujibu mwenyewe.

Wakili: Unafahamu lolote kwamba DPP alipata wapi ushahidi wa kumfikisha Zombe mahakamani?

Shahidi: Kutokana na maelezo ya Rashidi (mshitakiwa wa 11) na Rajabu (mshitakiwa wa 12) na maelezo mengine.

Wakili Maira: Uliwahi kuona ripoti ya Jaji Kipenka?

No comments: