Tuesday, January 13, 2009

PAROKO ANENA YA MKAPA MSIBANI

Wanasiasa walikuwepo!
Padre Claudio Kambili akishibisha waombolezaji na neno la Mungu

Wapendwa wakiwa wamebeba jeneza la Malima tayari kwa safari kuelekea Airport kwa ajili ya kuusafirisha leo asubuhi.
Paroko wa Kanisa katoliki Christ the King la Tabata jana amewasihi watanzania wamweheshimu Rais Benjamin Mkapa kutokana na menghi aliyoyafanya kwa ajili ya nchi.
Padre Claudio Kambili,alisema wakati wa misa ya kumuombea marehemu Cassian Malima aliyekuwa mhariri wa Habari Leo kwamba kitendo cha baadhi ya watu wakiwamo watoto wadogo kumzonga Mkapa kwa kumuita fisad ni kutomtendea haki rais huyo mstaafu ambaye wakati wa utawala wake wa miaka 10 aliwezesha kuupaisha uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya watu.
Akitoa mfano alisema mema mengi ya kiuchumi yakiwamo yale ya kuimarisha mfumo wa miundo mbinu ambao umeshuhudia kuwapo kwa barabara nyingi nzuri ambazo matundani yake yanawafaidisha Watanzania hadi leo hii, ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa na serikali aliyoiongoza Mkapa katika kipindi cha kati ya mwaka 1995 na 2005.
Katika ibada hiyo iliyohudhuriwa na umati mkubwa wa watu, wakiwamo viongozi wa serikali, vyama vya siasa, wanahabari na wananchi wa kawaida, Paroko Claudio alisema pamoja na ukweli kwamba Mkapa kama binadamu anayo mapungufu yake, lakini ukweli unabaki pale pale kwamba, wakati akiingia madarakani, hali ya uchumi wa taifa ilikuwa ni mbaya, kabla ya yeye kuiongoza serikali na kuiboresha.
‘‘Hivi sasa mambo haya yamesababisha hata wenzetu wa nje waanze kutucheka na kujiuliza hivi hawa ni wale Watanzania tuliowafahamu? Nchi inaelekea kubaya, hili suala la ufisadi, mtu mzima kama rais mstaafu Mkapa anaitwa fisadi...
Tunasahau kwamba Mkapa huyu alifanya kazi kubwa kuinua uchumi wa nchi...nasikia mtu anapita barabarani hata watoto wanapiga kelele fisadi huyooo! Tunakwenda wapi kama taifa?” Alihoji paroko huyo huku akiwaomba radhi waombolezaji waliofika hapo akisema anajua kwamba hapo hapakuwa sehemu sahihi ya kufikisha ujumbe wake huo.
Marehemu Malima atazikwa kesho huko Musoma mkoani Mara. Mungu Amrehemu, Amen

1 comment:

Anonymous said...

Huyu Paroko naona naye alikuwa kwenye payroll ya mkapa ndio maana anatetea.. Pambaf.

Kwanza watu wa didni inabidi waache kujihusisha na siasa.. haitakiwi..