Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na mkewe Tunu wakimpa pole mototo albino,Mtoba Malosa ambaye alinusurika kukatwa mkono wa kulia na watu ambao hawajafahamika nyumbani kwa wazai wake Njia Nne, Kashishi wilayani Urambo hivi karibuni.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda jana aliwaambia wananchi kuwa wanaoua watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) pamoja vikongwe hawana budi kuuawa kwa kuwa wakisubiri mahakama kuwahukumu, watakuwa wanakosea.
Waziri Pinda, ambaye ameanza ziara katika mikoa ya Kanda ya Ziwa yenye lengo la kuhamasisha vita dhidi ya mauaji ya vikongwe na albino, aliutaka Umoja wa Vijana wa CCM kuongoza vita hiyo, akisema lina jeshi zuri.
Mauaji ya albino yamekuwa ni tatizo kubwa nchini na hasa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa. Pamoja na serikali kutangaza hatua kadhaa za kupambana na wauaji hao, bado matukio ya kuuawa kwa watu hao wenye ulemavu wa ngozi yamekuwa yakiendelea kuripotiwa, lakini Waziri Pinda ameenda mbali zaidi katika kukabiliana na tatizo hilo alipotaka wauaji hao wauawe badala ya kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Kauli ya Pinda, ambayo inaweka maswali katika suala la utawala bora, imekuja wakati ambao wananchi wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi na kuua vikongwe kutokana na imani za uchawi.
Akihutubia wakati wa kufungua mkutano wa 16 wa Shirikisho la Vyama vya Kuweka na Kukopa (SCCULT) kwenye ukumbi wa Chuo cha Utumishi Umma mkoani hapa, Waziri Pinda alisema iwapo wananchi wataendelea kuwahurumia wauaji hao ambao wanatafuta viungo vya albino wakitegemea mahakama itatenda haki huku nao wakiongeza kasi ya mauaji kwa Watanzania, watakuwa wanakosea. Hivyo alisema kwamba kuanzia sasa mtu yeyote atakayemuona mtu amemkata shingo au mkono mweziwe basi naye auawe papo hapo hii itakuwa ndiyo dawa kwani vingozi wote tumechoka na mauji hayo. "Mkimuona mtu akamkata mwingine shingo naye muueni kwani sasa viongozi wote tumechoka... no more, I can't tolerate anymore (imetosha, siwezi kuvumilia tena)," alisema Pinda huku akiwaacha watu midomo wazi.
2 comments:
"Mkimuona mtu kamkata mwingine shingo, nae muueni" wamuue kwa kifo gani? maana wakimkata shingo itabidi nao wauawe. Pinda ni mwana sheria kitaaluma lakini ameshindwa kuelewa kuwa hata kumshauri mtu amuue mwingine ni kosa.
"...viongozi wote tumechoka." Hapa ndo angalau umenena....ni kweli ccm mmechoka
"Viongozi tumechoka"!!! Hivi mmeisha fanya nini kuhusu hili tatizo zaidi ya kuongea tu? Tatizo ni kwamba viongozi wetu bado wanaamini uchawi ndiyo maana wanaogopa kuwanyoshea vidole waganga wa kienyeji. Nasema hivyo kutokana na kituko cha unga Bugeni kilivyowangaisha wabuge.
Inabidi hatua za kisheria zichukuliwe kama vile kuwaprotect hawa ndugu zetu, watu inabidi waelimishwe kwamba utajiri unapatikana kwa kazi ngumu siyo short cut kama kuamini uchawi. Vyombo vya usalama (polisi) viwajibike kuwachukulia hatua kali wanaofanya vitendo hivi. Hukumu iwe ngumu kiasi kwamba wengine waogope kufanya vitendo hivyo. Inatia aibu kusikia Waziri Mkuu wa nchi kushindwa wajibu wake na kuwaachia wananchi wajichukulie sheria mikononi matokeo tutaanza kukatana mapanga kama wanyarwanda.
VIONGOZI WETU TAFADHALI ANZENI KUWAJIBIKA!
Post a Comment