Thursday, February 26, 2009

DEMOKRASIA CUF!!!!!!



SIKU mbili baada ya kuangushwa vibaya katika kinyang'anyiro cha uenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Abdallah Safari amesema wajumbe wa mkutano mkuu walimdhalilisha na kwamba anaandaa kitabu kueleza udhalilishaji huo.
Profesa Safari alitoa malalamiko hayo leo kuhusu matokeo ya uchaguzi huo uliomrudisha madarakani Profesa Ibrahim Lipumba, aliyepata kura 646, huku mpinzani huyo akiambulia kura sita tu.
Wakati Profesa Safari akijieleza, wajumbe walikuwa wakimzomea na baadaye kumrushia maswali yaliyomtingisha, ikiwa ni pamoja na kutaka ataje jina la katibu wa tawi lake, swali ambalo alibabaika kulijibu.
"Nimedhalilishwa; nimezomewa; nimeulizwa maswali ya kipuuzi. Ule ni uhuni hakuna kitu pale," alisema Profesa Safari.
"Wajumbe wa mkutano mkuu wa CUF wamepotosha na kuharibu maana ya demokrasia ndani ya CUF na kutumia vibaya nafasi hiyo ya kuchagua viongozi."
Alipobanwa kueleza iwapo anafikiria kuwania tena nafasi yoyote ya uongozi ndani ya chama hicho, Profesa Safari alisema hawezi na hana nia ya kuwania uongozi wa chama hicho.
"Sifikirii wala sina nia tena ya kuwania nafasi yoyote ndani ya CUF. Nitakapoita mkutano na waandishi wa habari, nitaeleza mengi. Mbali ya kuzindua kitabu changu, nitaamua shauli la kufanya pamoja na kesi ya uanachama wangu," alisema Profesa Safari.

No comments: