Tuesday, February 24, 2009

MAKUBWA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 24 Februari, 2009

“Hakuna Afisa wa CHADEMA aliyezuiwa kuingia kwenye ufunguzi wa Mkutano Mkuu”

Wapendwa Wanahabari,

Toleo la leo la gazeti la Majira limeandika habari iliyoitwa “Uhasama CUF, CHADEMA wazidi” huku likidai kuwa mlinzi wa Chama chetu cha Wananchi (CUF) alimzuia afisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuingia kwenye ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Nne wa Taifa wa Chama chetu jana.
Pamoja na kukanusha taarifa hiyo, tunaomba kuweka rekodi sawa. Kwanza Chama chetu kilivialika vyama vyote vya siasa, baadhi ya taasisi za kijamii, ofisi za kibalozi na jumuiya ya kiraia kushirikia katika ufunguzi huu kwa mwaliko rasmi. Kuna waliothibitisha kuhudhuria na waliothibitisha kutokuhudhuria kwa njia mbali mbali, yaani kimaandishi, kwa mawasiliano ya simu au ya moja kwa moja. Mmoja kati ya ambao walithibitisha kutokuhudhuria ni Katibu Mkuu wa CHADEMA, Mhe. Dkt. Wilbroad Slaa, ambaye aliongea moja kwa moja na Makamo Mwenyekiti wa Chama chetu, Mhe. Machano Khamis Ali walipokutana katika kikao cha Tanzania Center for Democracy (TCD) tarehe 19 Februari, 2009.
Wapendwa Wanahabari,
Wageni wetu wote waliohudhuria shughuli yetu ya ufunguzi walipokelewa na kutambuliwa rasmi kwenye Mkutano wetu na tunawashukuru sana. Hakuna kiongozi wala mwakilishi wa kiongozi yeyote wa CHADEMA ambaye aliwasili mbele ya walinzi wetu na kuzuiwa. Hiyo si sera wala msimamo wa CUF panapohusika mahusiano yetu na taasisi nyengine za kisiasa ama za kijamii. Hakuna uhasama wowote baina yetu na chama chochote cha kisiasa, CHADEMA ikiwemo, na hata kama panaweza kuwapo tafauti kati yetu na baadhi ya vyama vya kisiasa, utamaduni wa Chama chetu ni kuzizungumza tafauti hizo kistaarabu. Kwa mfano, kisiasa hakuwezi kuweko Chama cha siasa ambacho tunatafautiana sana kuliko Chama cha Mapinduzi (CCM), lakini washiriki wa Mkutano wetu ni mashahidi wa namna mwakilishi wa Chama hicho kwenye ufunguzi, Mhe. John Guninita, alivyopokelewa, kutambulishwa na kushangiliwa kwa heshima zote.
Wapendwa Wanahabari,
Tunaendelea kusisitiza kwamba sisi, CUF, ni chama cha siasa kinachofuata siasa za kistaarabu na kiungwana na kwamba tunajivunia utamaduni wetu uliotukuka katika nyanja hizo. Taarifa ya gazeti la Majira haikusema ukweli. Tunahimiza, kwa hivyo, uandishi unaozingatia utafiti, ukweli na unaozingatia maslahi ya pamoja ya taifa letu.
Pamoja na salaam za Chama.

Imetolewa na:
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba,
Mwenyekiti
The Civic United Front (CUF - Chama cha Wananchi)
P. O. Box 10979,
Ofisi Kuu - Dar es Salaam
Website: http://cuf.or.tz
Weblog: http://hakinaumma.wordpress.com

No comments: