Wednesday, February 11, 2009

Zombe amwaga chozi mahakamani, adai amesingiziwa

MSHTAKIWA wa kwanza katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka mjini Mahenge, Morogoro na dereva wa teksi wa Manzese jijini Dar es Salaam, Abdallah Zombe, jana alijitetea kwa zaidi ya saa tatu huku akimwaga machozi wakati akiwasilisha utetezi wake.

Zombe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) ambaye alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, alijikuta akimwaga machozi mara kadhaa wakati akijitetea mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, Salum Masatti kuhusu tuhuma hizo dhidi yake pamoja na askari wenzake tisa.

Hatua ya kupanda kizimbani jana na kuanza kujitetea ilikuja baada ya mahakama hiyo kuridhika kuwa, Zombe ambaye wakati wa mauaji hayo alikuwa akikaimu nafasi ya Kamanda wa Kanda ya Dar es Salaam, pamoja na wenzake, wana kesi ya kujibu kuhusu mauaji ya watu hao kulingana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.

Zombe, ambaye jana alisimama pia kama shahidi wa kwanza upande wa utetezi dhidi yake (Dw1), alibubujikwa na machozi wakati akitoa ushahidi wake na kujifuta kwa kitambaa mara kadhaa huku akigeukia pembeni.

Kutokana na kilio hicho cha kimya kimya, mara nyingine alijikuta akikabwa na kigugumizi cha uchungu kiasi cha kushindwa hata kuzungumza.

Akiongozwa na wakili wake, Jerome Msemwa katika utetezi wake uliochukua saa 3:38, Zombe alikanusha ushahidi wote uliotolewa mahakamani hapo kuwa si wa kweli na kwamba ulipangwa tu kwa lengo la kummaliza kwa sababu ambazo hata hivyo hakuweza kuzieleza.

Katika hali hiyo, Zombe alimtupia lawama Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuwa ni miongoni mwa watu waliohusika katika kupanga ushahidi kwa lengo la kummaliza katika hali ya kutapatapa baada ya kuona kuwa hawana ushahidi wa kumhusisha na tukio hilo.

Huku wakati mwingine akibishana na wakili wake katika namna ya kujitetea, Zombe alidai yeye hakuhusika na mauaji hayo kwa kuwa hakuwahi kuwafahamu marehemu hao kabla, wakati na hata baada ya vifo vyao.

Wakili Msemwa alikuwa akijaribu kumzuia kwa ishara wakati fulani, lakini Zombe alionekana kumbishia kwa ishara na wakati fulani kulazimika kuomba ruhusa kwa jaji ili aendelee kutoa maelezo yake.

Zombe alianza kwa kuieleza mahakama jinsi alivyokamatwa na kufikishwa mahakamani.

“Mimi nilikamatwa Juni 6 mwaka 2006 nikiwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi. Siku hiyo niliitwa kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Saidi Mwema na nilimkuta akiwa na makamishna wawili. Alikuwepo Kamishna Mtweve na Kamishna wa Mafunzo ambaye jina nimesahau," alidai Zombe.

IGP alinieleza kuwa leo ninaunganishwa katika kesi ya mauaji ya watu wanne, akaniambia kuwa mkurugenzi wa mashtaka ameleta barua kuwa niunganishwe katika kesi hiyo, kisha akanikabidhi barua hiyo,” alidai Zombe na kuitaja barua hiyo kuwa ni ya Juni 6 mwaka 2006.

Alisema barua hiyo, ambayo ilikuwa ikijibu barua ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) ya Mei 31 mwaka 2006, ilieleza kuwa, baada ya kukamilisha mambo kadhaa ya kiupelelezi na kwa ushahidi ulioko katika jalada tumefikia maamuzi kuwa, Zombe aunganishwe katika kesi hiyo.

“Sikubaliani na maelezo ya barua hiyo kwa kuwa ni ya kupangwa,” alidai Zombe akiongozwa na wakili wake.

“Barua hiyo ni ya tarehe 6/6/2006, DPP huyo huyo siku tatu kabla, yaani tarehe 3/6/2006, alikuwa amepokea barua kutoka kwa askari waliokuwa mahabusu katika Gereza la Ukonga ambao ni mshtakiwa wa tatu, mshtakiwa wa tano, mshtakiwa wa saba, mshtakiwa wa tisa na wa 10.”

Zombe alisema barua hizo, ambazo alizitoa mahakamani hapo kama kielelezo, zilikuwa zikienda kwa DPP na kwamba washtakiwa hao waliziandika kwa maelekezo ya DPP.

Zombe alidai kiutaratibu barua hizo zilipaswa zipitie kwa mkuu wa gereza na kwamba, ingawa zilionekana kuwa zimepitia kwa mkuu wa gereza, lakini ukweli ni kwamba zilikuwa zimepitia katika mlango wa panya.

“Naomba hii ya mshtakiwa wa tano niizungumzie kidogo na ninaomba busara za mahakama na za wazee wa baraza zitumike. Barua hii imeandikwa tofauti na nyingine zote kwa sababu mshtakiwa huyu anakaa Segerea (mahabusu). Bila shaka maelekezo ya DPP hakuyapata au aliyemfundisha hakumwelewa vema,” alidai.

Alidai baada ya barua hiyo ya DPP ndipo alipokamatwa ofisini kwa IGP mnamo saa 2.00 asubuhi na kwamba kufikia saa 2.15 alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Juni 9 mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Ady Lyamuya.

Zombe alisema siku ya mauaji hayo alikuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (RCO) na pia alikuwa Kaimu Kamanda wa Polisi akiwa na wasaidizi wapatao sita, katika nafasi ya kaimu RPC, wakati katika ofisi ya RCO alikuwa na wasaidizi watano.

Miongoni mwa wasaidizi hao wa RCO aliwataja kuwa ni Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Charles Mkumbo aliyekuwa mkuu wa kitengo cha ujambazi na uhalifu Dar es Salaam.

Kuhusu kuhusika katika tukio hilo, Zombe alidai siku hiyo alikuwa na shughuli maalumu ya kuongoza msafara wa Rais Jakaya Kikwete ambaye wakati huo alikuwa na ziara za kutembelea wizara mbalimbali na kutoa maelekezo ya utendaji na kwamba, majukumu yake aliyakabidhi kwa SSP Mafie.

Aliongeza kuwa, kwa nafasi ya RCO, jukumu hilo alilikabidhi kwa SSP Mkumbo na kwamba ingawa alikuwa na wasaidizi hao, walikuwa wakimwelezea yaliyokuwa yakitokea jijini, lakini wakati mwingine alikuwa akichelewa kurudi na hivyo alikuwa akienda nyumbani moja kwa moja.

Akielezea muundo wa Jeshi la Polisi, Zombe alisema kuna ngazi na madaraja mbalimbali ikiwa ni pamoja na wakuu wa polisi wa wilaya (OCDs) ambao ndio huwajibika kwa RPC na kwamba, hakuna sheria yoyote inayomzuia RPC kwenda katika kituo chochote cha polisi kwa kuwa vyote viko chini yake.

“Ushahidi uliotolewa hapa ni kwamba wewe ulikwenda katika kituo cha Polisi Urafiki, hebu iambie mahakama ni lini ulikwenda kama RPC na kwa nini?” aliuliza Wakili Msemwa.

“Kama Mtukufu Jaji alivyosema, hii ni moja ya sababu ya kunibakiza mimi katika kesi hii ili nisaidie kutoa ushahidi. Wasaidizi wa RPC ni OCD. Katika utaratibu wetu kama kuna tatizo kuna mawili ama kumwita aende mwenyewe au kumwita ofisini,” alijibu Zombe.

Hata hivyo, Zombe aliieleza mahakama kuwa siku hiyo alikwenda kituoni hapo baada ya kuitwa na OCD wa Magomeni, SSP Matage kuwa kuna tatizo ambalo alikuwa akihitaji msaada wake.

“Siku hiyo nilikuwa nimekwenda kumchukua mke wangu Hospitali ya TMJ katikati ya jiji. Dereva wangu aliyekuwa amebaki katika gari alikuja ndani akanitaarifu kuwa OCD Matage, alikuwa akiniita," alidai Zombe.

Nilikwenda tukaingia na mke wangu kwenye gari nikamuuliza OCD Matage, mahali alikokuwa akaniambia alikuwa Kituo cha Urafiki. Nilimuuliza alikuwa na jambo gani na kama kulikuwa na umuhimu wa mimi kwenda, akasema ilikuwa ni muhimu.”

Alisema walipofika ofisini walimkuta mkuu wa kituo hicho, SP Juma Ndaki, OCD Matage, SP Mkumbo, mshtakiwa wa pili, SP Christopher Bageni na mshtakiwa wa tatu, ASP Ahmed Makelle.

“Matage aliniambia kuwa hawa ofisa wa polisi (Bageni na Makelle) wanatoka kwenye tukio la uporaji wa pesa za Bidco ambako zimeokolewa Sh5,750,000, lakini Sh.1mil hazipo.. hapa kuna Sh4 milioni na bastola. Hawa ni maofisa wakubwa sasa nisaidie tufanyeje," alidai Zombe akimkariri Matage.

OCD alithibitisha Bidco wenyewe waliziona. Nilishangaa OCD kuniita kwa suala hilo ndipo nilimuuliza OCD kuwa kama ameshindwa kazi anithibitishie sababu haiwezekani kielelezo kikapotea na ndipo nilipokasirika na si vinginevyo nikatoa maelekezo kuwa nataka pesa hizo hizo zionekane kesho yake. Nikaondoka kwenda nyumbani kwangu.”

Alidai kwa kesho yake asubuhi mshtakiwa wa pili, Bageni alizipeleka na kumweleza kuwa zilipatikana kwenye gari. Asubuhi hiyo hiyo akawaita OCD wa wilaya zote, lakini ni askari wa chuo kikuu tu hakuwepo, ambapo walizungumzia hali ya uhalifu kwa kuwa wakati huo kulikuwa na ujambazi, watu walikuwa wakiuawa bila sababu.

Alidai walizumgumzia tukio la Bidco na kuwapongeza askari waliohusika kwa kuwatoa kimasomaso na kwamba pesa hizo zilifikishwa kwake na ndipo baadaye aliwaita waandishi wa habari ili kuwaeleza tukio hilo na kuwaonyesha fedha hizo na bastola hiyo.

“Tena nakumbuka gazeti la Mwananchi lilinionyesha nikiwa nimeshika hizo fedha na nikiwa nimeshika ile bastola. Fedha hizo pia zilifikishwa katika Tume ya Rais Kikwete,” alidai na kuongeza kuwa, OCD wa eneo husika pia aliandika taarifa ya tukio hilo.

Alidai taarifa za matukio yote huandaliwa tangu ngazi ya chini na kutumwa kwa viongozi wa juu hatua kwa hatua hadi kwa IGP kupitia katika mitambo maalumu na kwamba hata Ikulu kuna mtambo huo ambao ni mkubwa unaopokea matukio hayo yote.

“Hata zinapofika kwa RPC huzinakili kama zilivyo bila kuongeza ili kama likitokea jambo kama hili lililotuweka hapa, tunarudi kwenye taarifa hiyo,” alisisitiza.

Zombe alikanusha ushahidi wote hasa kuwa aliwavamia baadhi ya ndugu wa marehemu Muhimbili na kuwatishia na kwamba hata maelezo yao yanatofautiana jambo ambalo alisema linaashiria ushahidi wao si kwa kweli.

Zombe alidai ripoti ya tume ya polisi iliyoundwa kuchunguza tukio hilo ilikamilika tofauti na ilivyoelezwa na upande wa mashtaka na kwamba ilisainiwa na kupelekwa kwa IGP.

Alidai kuwa, taarifa hiyo haikumhusisha na tukio hilo, lakini kuna watu ambao hawakuifurahia. Alisema aliweza kuipata taarifa hiyo kwa kutumia mbinu zake kwa kuwa yeye ni mchunguzi na alikanusha madai kuwa alikataa kuandika maelezo na kutoa nakala ya maelezo yake aliyoyaandika Mei 29, 2006.


No comments: