Saturday, March 07, 2009

MAREHEMU ULEDI AZIKWA
MWANDISHI wa habari mwandamizi wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Michael Uledi amezikwa jana katika eneo la nyumbani kwao kijijini Buigiri.

Marehemu Uledi, ambaye hadi kifo kinamkuta alikuwa mwandishi wa habari kwenye kampuni hiyo inayochapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen, Mwanaspoti, Mwananchi Jumapili na The Sunday Citizen, akiwa mwakilishi mkoani Dodoma, alifariki juzi katika hospitali ya taasisi ya Mirembe alikokuwa amelazwa baada ya kusumbuliwa na ugonjwa wa kifua kikuu.

Mwili wake uliwasili majira ya saa 6:00 mchana na kufanyiwa ibada ya mwisho katika eneo la Buigiri Sokoni nyumbani kwa mama yake mdogo na baadaye kwenda katika eneo alilokuwa anajenga nyumba yake, ambako alizikwa katika kiwanja shamba lake.

Akitoa salamu za rambirambi katika eneo la makaburi, mhariri wa elimu wa Mwananchi, Joster Mwangulumbi alisema kuwa kampuni imempoteza mchapakazi na hodari na kwamba pengo lake haliwezi kuzibika kirahisi.

Mwangulumbi alisema kuwa kampuni ilimwamini Uledi kutokana na uchapakazi wake na sifa zake katika fani ya habari na ndipo ikaona hakuna kigugumizi cha kufanya uamuzi wa kumuajiri.

“Najua kama ingekuwa ni siku ya kuzaliwa kwake, tungekuwa na furaha kubwa, lakini leo tuna huzuni na kwamba pengo hili haliwezi kuzibika kwa familia na majirani na kwa kampuni pia,” alisema Mwangulumbi.


No comments: