Saturday, March 14, 2009

TANZIA MLOO

MLOO WA CUF ATUTOKA

The Civic United Front (CUF – Chama cha Wananchi) kinasikitika kuwaarifuni kwamba, leo asubuhi mwasisi wa chama hiki, Mhe. Shaaban Khamis Mloo, amefariki dunia, nyumbani kwake, mjini Zanzibar. Mazishi yake yanatarajiwa kufanyika leo leo saa 10.00 alasiri huko huko Zanzibar.
Marehemu Mzee Mloo alikuwa katibu mkuu wa kwanza wa CUF kwa miaka nane, kutoka 1992 hadi 2000 alipochukua nafasi ya umakamo mwenyekiti hadi alistaafu mwaka 2004. Yeye ndiye miongoni mwa waasisi wa Chama hiki, kwa kuanzia na vuguvugu la KAMAHURU. Ni yeye ndiye aliyeongoza mazungumzo ya kwanza na aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CCW), Mhe. James Mapalala, na hatimaye kuungana na kuzaliwa kwa CUF tuliyonayo sasa.
Kwa hivyo, CUF inamtambua Mzee Mloo sio tu kama kiongozi mstaafu wa Chama, bali zaidi kama mwasisi, mwanzilishi na mwanachama imara na shupavu katika siku zote za uhai wake. Atakumbukwa daima ndani na nje ya CUF kama mjuzi wa siasa za Zanzibar na za Tanzania kwa ujumla, mchapakazi na mtu aliyekuwa na ujasiri wa kupigiwa mfano.
Hata baada ya kustaafu umakamo mwenyekiti, Mzee Mloo aliendelea kuwa sehemu muhimu ya CUF kwa kujitolea katika mashauri mbali mbali. Kila alipokuwa na uwezo, hakuacha kuhudhuria mikutano ya hadhara au vikao vyovyote ambavyo alialikwa. Kikao cha mwisho kuhudhuria ni Mkutano Mkuu wa Nne wa chama chetu uliofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, kuanzia 23 hadi 27 Februari, mwaka huu. Kwa hivyo, hadi siku za mwisho mwisho wa uhai wake, Mzee Mloo alisimama imara kuijenga na kuihuisha CUF.
Wakati akiwaaga wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Tatu, Februari 2004, Mzee Mloo alitoa waraka, ambao pamoja na mengine ulikuwa na kauli ifuatayo:
“Nakuachieni Chama wjaumbe wote wa Mkutano Mkuu huu wa leo mukiwa na jukumu moja kubwa sana. Ingawa sisi tunastaafu, lakini tutaangalia kwa macho mawili utendaji wenu katika kata, matawi, majimbo, wilaya na taifa. Nakuachieni Chama kilichokamilisha theluthi mbili ya mtandao wake katika mikoa 26 ya Tanzania. CUF imeenea kila mkoa. Katika wilaya 130, CUF iko wilaya 117, katika vitongoji 38,000, CUF ina 20%, katika vijiji 11,600, CUF ina 15%. Mitaa yote 3,080, CUF ina 20%.”
Kwa hivyo, CUF iliyosimama leo hii kama taasisi imara ya kisiasa, imewezekana kuwa hivi kwa sababu ya juhudi kubwa zilizofanywa na Mzee Mloo na wenzake. Hakuna chochote tunachoweza kukifanya kukumbuka mchango uliotukuka wa Mzee wetu huyu, zaidi ya kutimiza ile ndoto yake ambayo daima aliishi nayo, yaani kuiona CUF kikiwa kinaongoza Serikali za Muungano na Zanzibar, kikitekeleza sera yake ya neema na haki sawa kwa wote.
Sisi tuliobakia nyuma yake, tunaahidi kwamba tutaitimiza dhamira na azma hiyo ya waasisi wa Chama hiki, akiwemo Mzee Mloo, kwa manufaa ya nchi na vizazi vijavyo. Tunaahidi kuwa CUF aliyoiasisi, kuijenga na kuisimamia kwa siku zote za uhai wake itaendelea kuwa taasisi imara ya kisiasa.
Katika wakati huu mgumu, tunaunganika na familia ya Mzee Mloo – hasa Mama yetu, Mama Mloo, na watoto wake – kumuombea dua. Mwenyezi Mungu ampokee mja wake akiwa ameshamsamehe makosa yake na aufanye mwema ujira wake. Amin.
Kwa heshima ya Mzee wetu huyu, mwasisi wa Chama chetu na kiongozi wetu mstaafu, Marehemu Shaaban Khamis Mloo, bendera zote za CUF nchi nzima zitapepea nusu mlingoti kwa siku tatu kuomboleza kifo chake.
HAKI SAWA KWA WOTE
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba,
Mwenyekiti

No comments: