Sunday, April 05, 2009

ATHUMANI HAMISI


Mpigapicha wa Magazeti ya Serikali, Daily News na Habari Leo, Athumani Hamisi aliyelazwa Hospitali ya Milpark nchini Afrika Kusini, ameishatoka katika hospitali hiyo kufuatia afya yake kuendelea vizuri ambapo sasa hapo amehamishiwa hospitali nyingine ya Medcare mahsusi kwa mazoezi ya viungo.
Mwandishi wa PPR aliyemtembelea Athumani Hamisi hospitalini hapo, alimshuhudia akifanya mazoezi ya viungo ikiwa ni pamoja na mazoezi ya kusimama kwa kwa msaada wa mashine maalum.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Athumani Hamisi amesema anaendelea vizuri ila amewaomba Watanzania wazidi kumuombea. Ametoa shukrani za dhati kwa Rais Kikwete aliyemtembelea mara mbili, pia anaishukuru serikali na mwajini wake kwa huduma zote anazopata ukiwemo ujumbe mahsusi toka Deily News ambao humtembelea kila mwezi.
Pia anaishukuru sana familia yake akiwemo mchumba wake aliyeko Nchini Marekani kwa jitihada zao kwake katika kipindi chote tangu kuugua kwake.
Mwandishi wa habari hizi, pia alimshuhudia Mwandishi mwingine wa Habari na Mtangazaji wa kujitegemea Pascal Mayalla aliyekuwa hospitalini hapo kufanyiwa uchunguzi wa Afya yake kufuatia ajali ya pikipiki mjini Dodoma iliyovunja mkono wake.
Mayala ambaye alishatibiwa nchini India, amesema anaendelea vizuri kwa mkono uliovunjika kupona japo bado umepoteza fahamu.
Wakati huo huo, habari ambazo hazijathibitishwa zinasema Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Rais, enzi za Mwalimu Nyerere, Mzee Tomothy Apiyo, pia amelazwa katika hospitali hiyo ya Milpark nchini Afrika Kusini. Taarifa kuhusu amelazwa tokea lini ama anasumbuliwa na ugonjwa gani, hazikuweza kupatikana.
Mwisho.


No comments: