Friday, May 29, 2009

MWAKYEMBE AJA JUU

Taarifa ya polisi yamkera Mwakyembe

Hii ni Taarifa yake kamili:

Nimesikitishwa na kufedhesheshwa na taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa Iringa Jumatatu iliyopita na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, James Kombe, na kutangazwa na vyombo mbalimbali vya habari kuhusu mazingira ya ajali ya gari niliyopata tarehe 21, Mei 2009, saa 1 na dakika 10 eneo la Ifunda, mkoani Iringa.

Taarifa hiyo ya Polisi inakanusha maelezo yangu yote na ya dereva wangu kuhusu ajali ilivyotokea na kunitaka nijiepushe kutoa matamshi kuhusiana na ajali hiyo kwa madai kwamba sina utaalamu na masuala ya ajali.

Taarifa hiyo nimeipata kupitia gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Mei 26, 2009 na kwa kuwa uwasilishwaji wake haujalalamikiwa na Jeshi la Polisi, naichukulia taarifa hiyo kuwa sahihi.

Pamoja na kwamba bado naumwa na niko nyumbani nikipumzika kwa ushauri wa madaktari, nimelazimika kuvunja ukimya na kutoa taarifa hii fupi kuzuia upotoshaji wa makusudi unaofanywa na magazeti, hususan gazeti la Tanzania Daima, na baadhi ya viongozi wa Jeshi la Polisi kwa sababu wanazozijua wenyewe kuhusu suala hili.

Aidha nataka kuelezea masikitiko yangu kuhusu hatua hiyo ya Jeshi la Polisi ambayo ina mwelekeo zaidi wa kisiasa kuliko utaalamu wa upelelezi na uendeshaji mashitaka kama ifuatavyo:

(1) Linapotendeka kosa, kazi ya Polisi ni kupeleleza na kukusanya ushahidi kwa lengo la kulifikisha suala husika kwenye chombo mahsusi cha utoaji haki, yaani Mahakama, ambacho kina utaalamu wa kuchuja ushahidi huo na kutenganisha uongo na ukweli ili kufikia maamuzi.

Hivyo hatua ya Polisi kuunda Kamati Maalum ya kupitia maelezo ya ushahidi niliyotoa na yale ya dereva wangu na kukusanya ushahidi wa ziada na baadaye kutoa uamuzi (nje ya mchakato wa kimahakama) kuwa ushahidi wangu na wa dereva wangu haukuwa sahihi, ni ukiukwaji wa mgawanyo wa madaraka wa vyombo vya dola au kwa maneno mengine ni uingiliaji wa mamlaka ya Mahakama kinyume na Katiba ya Nchi. Kitendo cha busara kingekuwa kutumia hayo wanayodai kugundua kwenye ushahidi mahakamani na siyo kwenye mkutano na waandishi wa habari!

(2) Uamuzi wa Kamati hiyo Maalum wa kumkamata na kumshitaki dereva wangu ambaye tayari Kamati hiyo imemhukumu mapema (pre-judged) kuwa mwongo na mzembe hivyo afunguliwe mashtaka mahakamani, hauendani na utawala wa sheria na misingi ya haki inayolindwa na Katiba na unaigeuza Mahakama kuwa chombo cha kupiga muhuri (rubber-stamp) maamuzi ya Polisi.

(3) Kabla na wakati ajali ikitokea mimi nilikuwa macho. Nasisitiza kuwa nimeshuhudia kila kitu mimi mwenyewe hadi nilipogongwa na kitu fulani kichwani na kupoteza fahamu.

Lakini Kamati hiyo Maalum inadai kwamba nilikuwa nimelala ati kwa sababu ningekuwa macho ningeliumia zaidi na kwamba walikuta kiti changu kimelazwa! Ningetegemea madai hafifu kama hayo kutolewa na mganga wa kienyeji anayetumia ramli kufanya maamuzi na siyo Jeshi la Polisi lenye utaalamu stahili, kwa sababu mbili kuu: Kwanza, safari yangu ilikuwa imeanzia Makambako ambako nililala, hivyo nisingeweza kuanza kusinzia baada ya safari ya karibu saa moja tu kutoka Makambako hadi Ifunda na kwenye mazingira ya baridi kali ya mwezi wa tano nyakati za asubuhi! Pili, gari lilipopinduka, kiti changu kiling’oka na kunifunika kwa mbele.

Hivyo nilitolewa sehemu hiyo kwa kukiiuna kiti hicho na kukilaza, jambo ambalo kwa Kamati hiyo maalum ulikuwa “ushahidi wa kitaalam” wa mimi kulala wakati wa ajali! Nadiriki kusema, hatua hii ya Polisi ya kutumia vyombo vya habari kukejeli ushahidi wa wahusika wakuu katika suala hili, yaani mimi na dereva wangu, ni kielelezo tosha cha jeuri na kiburi kisicho na tija wala maana cha baadhi ya viongozi kwenye vyombo vya dola waliolewa madaraka.

(4) Kwa kuwa sheria za nchi zinataka vyombo vya kiutawala vya maamuzi (quasi-judicial bodies) vizingatie kanuni za haki za asili (principles of natural justice), ni nini kiliizuia Kamati hiyo maalum kunihoji mimi na dereva wangu ili kukidhi matakwa ya kanuni za haki za asili na kupata picha iliyo kamilifu zaidi ya ajali hiyo?

Laiti mimi na dereva wangu tungelisikilizwa, nina uhakika kuwa taarifa ya Kamati hiyo maalum isingelisomwa kuchelea kulidhalilisha Jeshi la Polisi kwa kukosa umakini na viwango. Aidha nina mashaka makubwa kama Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, ambaye aliunda kamati hiyo maalum, aliiona taarifa hiyo ya Kombe mapema kabla ya kusomwa!

(5) Ajali ilitokea saa 1 na dakika 10 na muda mfupi baadaye RPC wa Iringa alidai na kunukuliwa na gazeti la The Citizen kesho yake kuwa chanzo cha ajali hiyo kilikuwa shimo la barabarani na kwamba ajali hiyo haikutokana na njama au hujuma zozote.

Msimamo wa RPC ulipingwa na kauli ya Meneja wa TANROADS, Iringa kuwa shimo lililokuwepo barabarani lilikuwa dogo mno kuweza kusababisha ajali ya gari aina la Land Cruiser lenye mataili makubwa. Maswali yangu ni matatu: Kwanza, nini kilimsukuma RPC muda mfupi baada ya ajali hiyo kutokea na hata kabla ya kuwahoji majeruhi, kutoa tamko la kwamba chanzo cha ajali kilikuwa shimo?

Pili, nani aliyemwambia RPC kuwa ajali hiyo ilitokana na hujuma au njama kiasi cha yeye kulazimika kutoa tamko gazetini mapema kama alivyofanya? Tatu, Kamati hiyo maalum ilibaini sababu zipi za msingi za RPC na Meneja wa TANROADS kutofautina juu ya chanzo cha ajali?

(6) Katika gazeti la Tanzania Daima, toleo la Jumapili, tarehe 24 Mei, 2009, dereva wa lori (ambaye mimi na dereva wangu tulimtaja kwenye maelezo yetu ya maandishi) amenukuliwa akisema yafuatayo: kwamba hakuligonga gari langu kwamba dereva wangu alikuwa mwendo wa kasi na alikuwa mzembe na kwamba Polisi walikuwa wanaunga mkono kauli ya dereva huyo. Maswali yangu ni matatu tu:

Ni nini kiliizuia Kamati hiyo maalum na hadi sasa kinalizuia Jeshi la Polisi kumhoji vizuri dereva huyo wa lori kupitia kwa mwandishi wa Tanzania Daima?

Pamoja na kuchelewa sana, Polisi wanaogopa nini kulikamata lori hilo na kulikagua kujua kama lina alama ya kulikwangua gari langu? Kwa nini Polisi wanakwepa kabisa kulitaja lori hilo kwenye taarifa zake wakati wananchi walioshuhudia ajali hiyo na askari mmoja wa usalama barabarani waliliona likiwa sambamba na gari langu kwa muda kabla ya ajali kutokea?

(7) Katika toleo hilo la Tanzania Daima, dereva huyo anadai kuwa aliiona ajali ikitokea mbele yake, lakini hakusimama, akaendelea na safari yake. Ni nini tafsiri ya wataalamu wa Kamati hiyo maalum kuhusu kitendo hicho?

(8) Taarifa ya Kamati hiyo maalum ya IGP inaoana kwa kila hali na taarifa mbalimbali zilizochapishwa na gazeti la Tanzania Daima toka ajali itokee, kiasi ambacho taarifa ya Kamati hiyo maalum ingeweza kuandikwa (bila hata Kamanda Kombe na wenzake kuchoma mafuta kwenda Iringa) kwa kutumia taarifa za gazeti hilo tu.

Ni nini uhusiano wa baadhi ya viongozi wa Jeshi la Polisi na gazeti hili? Ni nini uhusiano wa lori hilo na gazeti la Tanzania Daima na/ au viongozi wa Polisi Iringa?

(9) Taarifa ya Kamati hiyo maalum, kwa mujibu wa gazeti la Tanzania Daima la tarehe 26 Mei, 2009 inanitaka nisitoe kauli zisizo za kitaalamu! Nina maswali kadhaa ya kuuliza: Kwanza, ni utaalamu gani unahitajika kuelezea kitu kilichomsibu mtu?

Mathalan, nyumba yangu imeungua moto. Kwa mantiki ya kamati hiyo maalum, siruhusiwi kuelezea kuwa chanzo cha moto kilikuwa kibatari au mshumaa, mpaka nimsubiri Kombe na timu yake ya “wataalam” waje kupiga ramli kama walivyofanya kwenye ajali yangu?

Pili, tumepata ajali nyingi nchini na abiria na madereva wamekuwa chanzo muhimu cha taarifa kwa Polisi kujua chanzo cha ajali. Kwa nini vigezo na taratibu zigeuke kwenye ajali ya Dk. Mwakyembe peke yake (ambapo wahusika wakuu katika ajali hiyo hawatakiwi kuongea)? Tatu, kama suala hapa ni uelewa wa sheria husika, mwenendo wa upelelezi na wa mashitaka, ni nani katika Kamati hiyo ya Kombe anayeweza akadai kuwa na uelewa mpana na wa kina kunipita?

(10) Tumepata ajali nyingi kama Taifa zilizosababisha majeraha na vifo vya wananchi na viongozi na hata kuzua maswali mengi kuhusu vyanzo vya ajali hizo bila Polisi kuingilia uhuru wa kusema wa majeruhi wala kuunda Kamati maalum za uchunguzi.

Lakini ajali yangu ambayo kwa ulinzi na baraka za Mwenyezi Mungu haijasababisha upotevu wa maisha, inajengewa kwa makusudi mazingira ya malumbano na kuundiwa Kamati maalum ya uchunguzi yenye lengo la kuziba watu midomo. Hamasa hii ya Jeshi la Polisi kudodosa kila ninalolisema na kulitafutia maelezo mbadala, inatokana na nini, inachochewa na nini na kwa faida ya nani?

Nimalizie kwa kusema mambo matatu ya ziada, kwa kifupi sana. Kwanza, mtu yeyote mwenye akili timamu, hawezi kutetea uzembe wa dereva wake maana kwa kufanya hivyo, atakuwa anajichimbia kaburi lake mwenyewe! Vivyo hivyo, mtu yeyote muungwana hawezi kukubali au kuridhia mtu mwingine kutuhumiwa uwongo. Hiyo ni dhambi.

Pili, Jeshi letu la Polisi ni chombo muhimu sana cha ulinzi na usalama kinachobeba imani kubwa ya wananchi wote bila ubaguzi. Kamwe kisiingizwe kwenye siasa na daima kizingatie haki na kionekane kinazingatia haki kwa misingi ya sheria na Katiba ya Nchi.

Tatu na mwisho, ilipotokea ajali kauli yangu ya kwanza ilikuwa: hii ni ajali ya kawaida, na yote namwachia Mwenyezi Mungu. Lakini purukushani hizi za Polisi za “funika kombe mwanaharamu apite”, zinanifanya niingiwe na wasiwasi kuwa ajali yangu haikuwa ya kawaida. Pamoja na wasiwasi huo, bado namwachia Mwenyezi Mungu mwenye maamuzi ya mwisho.

10 comments:

Anonymous said...

HAKUKUA NA SABABU YOYOTE KUUNDWA KAMATI KUCHUNGUZA TUKIO, HUU MTINDO WA AJALI IKITOKEA NA ENDAPO DEREVA HAKUWA KIONGOZI BASI HUCHUKULIWA KAMA HUENDA KUNA NJAMA SI SAHIHI. TULISHUHUDIA AJALI YA KIONGOZI ILIWAHI KUTOKEA NA DEREVA ALIKUWA MKE WAKE, HAIKUUNDWA KAMATI KWANI ILIONEKANA KUWA NI AJALI YA KAWAIDA, LAKINI DEREVA ANGEKUWA WA KUAJIRIWA AJALI HIYOHIYO INGEONEKANA KUWA NA MASHAKA! HII INAONESHA AJALI SASA KUINGIZWA KWENYE SIASA.

Anonymous said...

Lakini hapa kauli ya passenger (Mwakyembe)na dereva wake ni moja kwamba kuna lori iliyoigonga gari yao. Polisi na tume yao hawataki kuelewa wanamuangukia dereva wa Mwakyembe tu. Polisi hawataki kumtafuta dereva wa lori wala hawana taabu kama huyo dereva akiendelea kutoa taarifa kwenye vyombo vya habari bila kupigwa picha na bila kutajwa jina!!Lakini Kombe (mkuu wa trafic police)anamuonya Mwakyembe asizungumzie hiyo ajali kwenye vyombo vya habari.Na yeye mwenyewe na PPC wa Iringa msatri wa mbele kabisa kuzungumzia hii ajali kwenye vyombo vya habari na kumfanya mbunge eti mwongo.Polisi inaficha kitu hapa (mkono wa fisadi?)!!

Ajali zingine kama za Mbatia na Sokoine na Chacha Wangwe mbona hazikuwa na tume? Mbona ulifanyika uchunguzi wa kipolisi ukapelekwa mahakamani bila Public Relatons kibao na mikutano na vyombo vya habari kwa wingi na RPC na tume. Polisi wanataka kutuaminisha kitu cha kutunga kabla hata ya kwenda mahakamani.Wamechelewa tuko macho na hawaaminiki

Anonymous said...

Pole Mheshimiwa Dr. Mwakyembe. Hata hivyo, nadhani mazingira haya ya ufuatiliaji wa mambo yanayokupa shaka hata kuhitimisha maelezo yako kwa kulitaka Jeshi la Polisi lisiingizwe kwenye siasa ndiyo limekupambanukia leo? Au paka likukute binafsi ndpo ujue kwamba ndivyo mambo yalivyo?

Anonymous said...

Mheshimiwa anonymous wa tatu: Lakini unajua Mwakyembe anaitwa CHADEMA na wabunge wanamtandao wa CCM?? Kwa hiyo maoni yake haya hayashangazi. Japo kuwa yuko chama tawala maoni yake mengi huyu bwana si ya kinafiki na yanatetea kuheshimiwa kwa sheria. Si swala la ufisadi tu na polisi kutoshiriki katika siasa. huyu mbunge kwenye jimbo lake anapata joto ya jiwe kutokana na kushinikizwa na vyombo vya dola na wanamtandao.

Anonymous said...

Hivi mbona Chenge alizungumzia ajali yke kwa uhuru tu bila tume kumwambia asizungumze na magazeti. Hivi wewe Kombe una nini wewe? Kwa nini unatoa kauli za ajabu ajabu? un nini wewe? Eti Mwakyembe asizungumzie mabo asiyo na ujuzi nayo.

Anonymous said...

SINA IMANI NA KOMBE

John Mwaipopo said...

Kombe keshajiingiza kwenye siasa. kama sio siasa basi amejiingiza kwenye upiga ramli. Hivi mie niko kwenye gari naendeshwa kilometa sema 100 kwa saa, napata ajali, gari linaumia,halafu mtu aliye dar es salaam anajua fika kuwa nililala au nilikuwa macho.

Anonymous said...

Sasa sikilizeni vituko vya wakubwa kutoka www.francisgodwin.blogspot.com
wakati ripoti haijamfikia aliyeiunda tume, wakati polisi wakijikanyaga kuhusu ripoti ya Kombe na kuiita eti si rasmi na ripoti rasmi bado haijatolewa Njelu Kasaka na Mrema wanasema hivi:
"Aliyekuwa mbunge wa jimbo la Lupa ,Mbeya (CCM) Bw Njelu Kasaka kulia akisalimiana na waziri wa Afrika Mashariki Dr Diodorus Kamala katika chuo cha Tumaini leo


Bw Kasaka na mwenyekiti wa TLP Taifa Bw Mrema wametoa maoni yao juu ya utata wa ajali ya DR Mwakyembe


Mrema asema lazima iundwe tume nyingine huru chini ya waziri wa mambao ya ndani ili kuchunguza utata wa ajali hiyo vinginevyo suala hilo linakoelekea ni kubaya zaidi .

Huku Bw Kasaka asema ana imani kubwa ya tume iliyoundwa kuchunguza suala hilo........"

Sasa Mrema anataka tume nyingine tena chini ya wizara hiyo hiyo iliyoshindwa na tume ya kwanza. Alafu wizaa yenyewe ina maskandali kibao tenda ya vitambulisho vya uraia, vinasa sauti kwenye chumba cha Dk. Slaa, wageni na hata waliopigwa marufuku kuishi na kurudi nchini kinyemela (Chavda). Si jamani ungozi wa wizara hii unaonekana umeshindwa, Mrema anataka iendelee tena kuboronga na tume nyingine??

Ndugu yangu Kasaka eti ana imani kubwa na tume wakati Mwakyembe (gwiji wa sheria) kawaorodhoshea dosari kumi za utaratibu za tume hiyo na tume imeshindwa kujibu na badala yake Polisi inasema ripoti aliyoitoa Kombe si rasmi, kana kwamba kazi bado. Sasa mbona Kombe alipotoa taarifa alikua anatuambia amemaliza. Sasa imani ya Kasaka na kitu kibovu, ambacho hata IGP aliyeunda tume anshindwa kukikumbatia, inatoka wapi?

Jamani ee njaa hizi za viongozi wachovu zinawasababisha kubugia mpunga wa Rujewa nini? Wanashindwa kugfikiri kabla ya kutoa kauli.Lakini hii ndiyo mbinu ya mafisadi kuwatumia anasiasa wa zamani wachovu kuwasemea hoja zao. Maana hawa hawtasita kupayuka mradi kuna tugunia tuwili, tutatu twa mpunga tunapatikana kutoka Rujewa!!

Anonymous said...

kombe kafuliiiia tena na mbuni

Anonymous said...

Chenge alikuwa huru kujieleza tena uku akiwa analindwa na lundo la askari. mbona hakuambiwa akae kimya? ipi ajali mbaya kati ya chenge na mwakyembe?
Mtu ameua na bado yupo huru!! wewe kombe unamtafuta nini mwakyembe?
Polisi acheni kujiingiza katika siasa fanyeni kilichocha wajibu wenu. mengine waachieni wenyewe.