Friday, May 29, 2009

ULIMI WAZUA BALAA


Mahakama yavunja ndoa ya mwanamke aliyemn’gata ulimi...


MAHAKAMA ya Mwanzo Buguruni jana ilivunja ndoa ya Deogratus Sangu (34) na Joyce Msilanga (28),baada ya kuridhika kwamba kitendo cha Joyce kumng'ata ulimi mwanaume mwingine wakiwa kwenye penzi ni cha aibu.
Hivi karibuni, kituo kimoja cha televisheni kiliripoti kwamba mwanaume mmoja (jina linahifadhiwa) wa Jiji la Tanga aling'atwa ulimi na mwanamke baada ya kunogewa na penzi.
Kamanda wa Polisi mkoani Tanga alidai mwanamke huyo alimng'ata mwanaume ambaye siye wake akiwa kwenye nyumba ya kulala wageni .
Kufuatia tukio hilo, mumewe Joyce ,aliamua kwenda mahakamani kufungua kesi ya kuomba kuvunjwa kwa ndoa yao kwa kuwa mkewe amemdharilisha kwa ndugu, jamaa na marafiki zake.
Ombi hilo alilifikisha Mei 13 mbele ya Hakimu, Jamila Massengi kutokana na tukio hilo la aibu ambalo alidai hawezi kulivumilia kwa hali yoyote.
Mkewe alipoitwa mahakamani na kuulizwa kama aliridhika na maamuzi ya mumewe, alikubaliana na maamuzi hayo na kutaka wagawanyishwe mali walizopata wakati wa ndoa yao iliyofungwa Kikristo mwaka 2003 na kujaliwa kupata mtoto mmoja.
Ndipo mahakama ilipoanza kusikiliza maelezo ya kila moja hadi kufikia uamuzi wa kuvunjwa kwa ndao yao na iliamua wagawane mali ambazo walipata wakiwa ndani ya ndoa na kuamua mtoto abaki kwa Sangu kwa kuwa mwanamke huyo hana kazi.
Awali, mumewe huyo alidai mahakamani hapo kwamba aliamua kumpeleka mkewe mkoani Tanga kwa ajili ya masomo ya ualimu katika chuo cha Kange, lakini badala ya kusoma alitenda kosa na hakuweza kumaliza masomo yake jambo lililomfanya arejee jijini Dar es salaam.

No comments: