Wednesday, August 26, 2009

CHADEMA MAMBO!!

Zitto afafanua hamu ya kumg'oa Mbowe Chadema

NAIBU katibu mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe amesema ana sababu za msingi za kuamua kuuwania uenyekiti wa chama hicho, huku mwenyekiti wake Freeman Mbowe akimkaribisha katika kinyang'anyiro hicho.

Zitto, ambaye yuko nchini Ujerumani kikazi, aliiambia Mwananchi jana kwamba, ameamua kuingia katika kinyang’anyiro cha uenyekiti kupambana na Mbowe kwa lengo la kuandaa chama kuchukua dola.

Lakini Mbowe, ambaye uongozi wake umeifanya Chadema kuwa tishio kwa chama tawala na upinzani, alisema anamkaribisha mwanasiasa huyo kijana katika kuwania nafasi hiyo, akisema uamuzi huo ni haki ya kila mwanachama wa chama hicho kugombea nafasi yoyote kama ana sifa.
“Sina mengi ya kusema; kama alivyosema Dk Slaa (Willibrod) kila mwanachama anaruhusiwa kugombea nafasi yoyote, hivyo sina tatizo na Zitto kuwania nafasi hiyo,” alisema Mbowe.

Zitto, ambaye ameibukia kuwa mwanasiasa maarufu mwenye uwezo wa kujenga hoja, alisema anatambua kazi nzuri ambayo Mbowe ameifanya katika chama, lakini akaongeza kuwa, uamuzi wa kupambana naye unalenga kukiandaa chama kuchukua dola katika chaguzi zijazo.

“Ninajua kazi ambayo Mwenyekiti Mbowe kaifanya kwenye chama. Ni kazi kubwa sana na hata mimi kuwepo kwangu katika siasa, Mbowe amechangia sana, alisema Zitto ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 32.

“(Mbowe) Ni kiongozi ninayemheshimu na kwa kweli anakipenda sana chama na amejitolea sana kwa ajili ya chama.”

Hata hivyo, Zitto, ambaye aliwahi kukaririwa akisema nia yake siku moja ni kushika nafasi ya juu ya uongozi katika nchi akimaanisha urais, alisema ni lazima chama kionekane sasa kipo tayari kuchukua dola.

“Mbowe ni kiongozi mzuri sana wa chama ambacho kipo katika siasa za upinzani. Watanzania sasa ni lazima wapewe sera mbadala za kuonyesha kuwa tunaweza kutawala. Jambo la msingi kuliko vyote ni kuona chama kinabaki kimoja na imara. Hili ndilo lengo langu,” alisema.

Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini ambaye alijiunga na Chadema akiwa na umri wa miaka 16, alisema ingawa katika uongozi wa Mbowe amekuwa na mafanikio, chama hicho kimekuwa katika hali ya kufukuza wanachama.

“Tumefukuza sana wanachama. Haiwezekani tukajenga chama cha kufukuzana tu. Ni lazima tukubali kutokubaliana,” alisema.

“Kugombea kwangu ni wito wa kurejesha umoja katika chama wakati tunajiandaa kuchukua dola. Uchaguzi Mkuu wa 2010 utakuwa wa kihistoria kwa kuwa kwa uzoefu wangu unaweza kulazimisha serikali kuundwa na waziri mkuu ambaye hatoki CCM. Hatuwezi kwenda huko tukiwa divided (tumegawanyika).”

Akielezea mafanikio ya Mbowe, Zitto alisema mwenyekiti huyo ameiwezesha Chadema kutoka kupata asilimia tatu ya kura katika uchaguzi wa mwaka 2000 mpaka asilimia 8 mwaka 2005.

“Tunamshukuru kwa kukiimarisha chama chetu. Sasa ni wakati wa chama kuelekea kushika dola. Lazima kukiandaa chama kushika dola,” alisema Zitto.

“Hiyo ndio kazi ambayo nimeombwa kuifanya na wana-Chadema mikoani na wilayani. Hii ndio kazi ambayo kwa moyo mzito nimekubali kuifanya.”

No comments: