Friday, February 19, 2010

ZUNGU MANARA KWISHA!!!


ALIYEKUWA Katibu Mwenezi wa CCM, mkoani Dar es Salaam, Haji Manara (35), jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kujibu mashtaka sita ya kujipatia mali na fedha kwa njia ya udanganyifu.
Alipandishwa kizimbani saa 7:45 mchana na kusomewa mashtaka hayo mbele ya hakimu mkazi Benadictor Beda.Mwendesha mashtaka Batseba Kasanga alimwambia hakimu Beda kuwa katika shtaka la kwanza mtuhumiwa aliiba gari aina ya Toyota OPA mali ya Abdul Ngalawa.Kwa mujibu wa Kasanga tukio hilo lilifanyika Novemba 27 mwaka jana eneo la Magomeni jijini Dar es Salaam.
Mwendesha mashtaka huyo alifafanua kuwa katika tukio hilo, mtuhumiwa alipewa gari hilo na mlalamikaji ili akaiuze kwa Sh10 milioni na kumpa fedha hiyo lakini, baada ya kuiuza, hakumpelekea fedha wala kumrudishia gari yake.
Kasanga alizidi kudai mahakamani hapo kuwa Desemba 19, mwaka jana, kwa njia ya ulaghai, mtuhumiwa alijipatia magari mawili yenye namba aina ya Toyota IPSAM na Toyota NADIA mali ya Asma Miraji.Alisema mtuhumiwa alipewa magari hayo kwa makubaliano kuwa angeyarudisha baada ya siku kumi lakini, hakufanya hivyo.
Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka huyo, katika shtaka lingine Manara alijipatia pia Sh5 milioni kutoka kwa Jocob Manyanga kwa makubaliano kuwa angemuuzia gari lake, kitu ambacho hakufanya.Alisema tukio hilo lilitokea Januari tano mwaka huu manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Kasanga alimweleza hakimu Beda kuwa Desemba 20 mwaka jana, eneo la Magomeni mtuhumiwa huyo alijipatia tena Sh3 milioni kutoka kwa Wilson Matimba kwa makubaliano ya kumuuzia gari yake.Alisema pia Januari 29 mwaka huu eneo la Magomeni saa 11:00 jioni, Manara alijipatia Sh19 milioni za mkopo kutoka kwa Dotto Hussein akieleza kuwa yeye ni mfanyabiashara na kwamba angemrudishia fedha hiyo baada ya siku tano.
Mwendesha mashtaka huyo aliendelea kudai mahakamani hapo kuwa Manara pia alijipatia Sh36 milioni kutoka kwa Fadhili Mtandika mkazi wa eneo Magomeni jijini Dar es Salaam kwa njia ya utapeli.Alisema mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Januari 13 mwaka huu saa 2:00 usiku.
Hata hivyo mtuhumiwa huyo alikana makosa yote sita na kurudishwa rumande kwa kukosa dhamana hadi Machi 4 mwaka huu kesi hiyo itakapoendelea.
Mtuhumiwa aliswekwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni pamoja na kuwa na wadhamini wawili wanaofanyakazi zinazofahamika, wawe na mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh 35milioni au fedha tasilimu Sh 17milioni.

No comments: