Thursday, January 13, 2011

INDIA KUWEKEZA NCHINI 375 BILIONI

WAWEKEZAJI kutoka India wameonyesha nia ya kutumia zaidi ya Sh375 bilioni kwa ajili ya kujenga viwanda saba vikubwa nchini vya bidhaa mbalimbali vitakavyotoa ajira zaidi ya 6,000.

Akizungumza jijini Dar es Salaam baada ya kumaliza ziara yake nchini India, Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk Cyril Chami, alisema ziara hiyo imekuwa na mafanikio makubwa na wawekezaji wengi kutoka nchi hiyo wametamani kuanzisha biashara zao nchini.


Dk Chami alisema kampuni kubwa ya chuma nchini India, Kamal Steel Industries, inataka kuwekeza kiwanda kikubwa kwa gharama ya Sh30 bilioni na kutoa zaidi ya ajira 5,000 nchini.


“Sisi tulikuwa tunatafuta watu wenye mitaji na wenye teknolojia ili waweze kuwekeza nchini, Watanzania wapate ajira. Watu wakiwa na ajira tunapunguza hata uhalifu,” alisema Dk Chami.


Alisema Kampuni ya Kamal Steel tayari imewekeza nchini kiwanda cha aina hiyo kilichoko Barabara ya Nyerere ambacho ni kidogo na kimetoa ajira kwa Watanzania 400.


Waziri huyo alisema licha ya kiwanda cha chuma kujengwa nchini, kampuni inayotengeneza Bajaj imekusudia kuweka kiwanda cha kuunganisha magari na pikipiki za kampuni hiyo ambacho kitagharimu Sh30 bilioni na kutoa zaidi ya ajira 400.



Katika msafara wake, Dk Chami aliongozana na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitillya , Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji EPZA, Adelhelm Meru na Ofisa Mtendaji Mkuu wa TanTrade, Ramadhan Khalfan.



Alitaja miradi mingine iliyopatikana kuwa, ni Kiwanda cha mbegu bora ambacho kinatengenezwa na kampuni nyingine ya India inayofahamika kama Science and Corp Limited itakayowekeza kama dola za Marekani 3 milioni na kutoa zaidi ya ajira 500.



“Kiwanda kama hiki ni muhimu kwetu kwa sasa hasa ukizingatia kuwa, serikali imetia mkazo katika kilimo kwanza na ukiangalia vyote hivyo vitasaidia kuendekleza na kuboresha kilimo chetu,” alisema Waziri Chami.



Dk Chami alitaja Kampuni ya UK Electrical ambayo inatengeneza vifaa mbalimbali vya umeme kuwa, nayo itawekeza nchini na kwamba, kampuni nyingine ya Lotters Packaging Ltd itajenga kiwanda cha upangaji bidhaa kwa kuwekeza dola 1.2milioni za Marekani.



Viwanda vingine ni UK Electrical kitakachukuwa kikitengeneza pampu za maji na majenereta na kuwa, kuna kampuni nyingine ambayo imeanza mazungumzo kwa ajili ya kutengeneza teknolojia ya vipuri na mashine ndogondogo.

“Sasa huyu wa mwisho namuona ni muhimu kwa kutengeneza mashine ndogondogo atasaidia wajasiriamali wa pale gerezani kwa kuwapatia mashine na vipuri,” alisema.

No comments: